Close

Not a member yet? Register now and get started.

lock and key

Sign in to your account.

Account Login

Forgot your password?

MAHOJIANO YA JANUARY MAKAMBA NA JARIDA LA ‘UMOJA’ August 2010 Issue 001

 

1. Umekuwa msaidizi wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete tangu akiwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa hadi hivi sasa, ni mambo gani hasa umejifunza kutoka kwake?

  Nimejifunza mambo mengi sana kiasi kwamba ni si rahisi kuyazungumzia yote katika muda huu mfupi. Lakini, kwa kifupi, nimejifunza kutoka kwake kwamba falsafa sahihi ya uongozi ni kuongoza kwa mfano. Rais Kikwete anafanya kazi kwa bidii kuliko watu wote anaowaongoza na ni muadilifu kuliko watu wote anaowaongoza. Kwahiyo anapozungumzia bidii ya kazi, ni rahisi kumuamini na kumfuata. Anapungumzia maadili, unajua kabisa kwamba hazungumzi kwasababu ya siasa. Anazungumza maadili kwasababu yeyé ndio maisha yake anayoishi na ni rahisi kumuamini na kumfuata. Pia nimejifunza kutoka kwake kuhusu umuhimu wa subira, uungwana, na utu. Rais Kikwete anajiamini sana na anaamini katika uwezo wake na katika dhamira yake njema kwa nchi kiasi kwamba hasumbuliwi na maneno maneno au matukio ya pembeni. Amenifundisha kwamba kama unaamini katika unachokifanya na kama unamiini katika nia yako njema, maneno ya pembeni na matukio ya kupita hayapaswi kukuondoa kwenye malengo yako ya msingi. Nimejifunza kutoka kwake kuhusu umuhimu wa tafakuri ya kina kabla ya kufanya maamuzi au kutoa matamshi, kwamba hata kama kuna shinikizo kubwa kuhusu uamuzi au hatua fulani, kama unashika nafasi ya dhamana kubwa, ni muhimu kutafakari kwa kina na kutafuta maelezo, ushahidi, vielelezo na ushauri na kujiridhisha kabla ya kufanya uamuzi. Pamoja na yote hayo, nimejifunza kutoka kwake kwamba siasa ni nyenzo ya utumishi wa umma sio fursa ya kujinufaisha wala kutafuta umaarufu.

  2. Unaweza ukalieleza jarida hili ni kwa namna gani hasa ulipata fursa ambayo hatimaye ilikukutanisha na rais Kikwete?

  Kwanza wakati nasoma nilipata fursa ya kufanya mazoezi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa kipindi cha miezi mitatu, ambapo nilikutana na Waziri Kikwete mara kwa mara, hasa katika mikutano pale Wizarani. Karibu kila siku nilikuwa naandika uchambuzi wangu kuhusu masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Tanzania. Naamini baadhi ya uchambuzi wangu ulikuwa unamfikia. Baada ya kumaliza shahada yangu ya pili, niliomba kazi Wizarani na nikafanikiwa kupata. Kwasababu ya mambo niliyosomea, nilibahatika kufanya naye kazi kwa karibu, hasa wakati ule akishughulikia mgogoro wa Burundi. Nilikuwa sisiti kuandika mawazo na uchambuzi wangu kuhusu masuala mbalimbali tuliyokuwa tunashughulika nayo kama Wizara. Nadhani aliona uwezo wangu, kwahiyo alipoamua kugombea Urais akanitaka niwe Msaidizi wake wakati wa Kampeni. Nikabahatika kuzunguka naye nchi nzima, nikimsaidia kuandika notes zake kila anapohutubia na kuhakikisha mambo yanaenda vizuri kwenye safari zake za kampeni. Alipofanikiwa akanipa heshima ya kuwa mmoja wa Wasaidizi wake hapa Ikulu.

  3. Je ukijipima, unadhani umefanikiwa kutimiza wajibu wako sawia wa kumsaidia rais Kikwete wakati wote ulipofanya kazi naye?  

Hili ni swali la Rais mwenyewe. Ninachoweza kusema tu ni kwamba nimejitahidi kwa kadri ya uwezo wangu. Mimi ni binadamu, na ninazo kasoro kwahiyo siwezi kusema kwamba nyakati zote nilifanikiwa kukidhi matarajio yake. Lakini hata siku moja sikusahau kwamba kumsaidia Rais ni heshima kubwa, ni fursa ya kushiriki kutengeneza historia ya nchi, na imani ya Rais kwangu ni jambo ninalolichukulia kwa uzito mkubwa; imani ya Rais ni jambo linalompa mtu heshima kwenye jamii. Siku zote sikusahau na sitasahau kwamba nina deni kubwa kwake. Kwa maana hiyo, hata pale nilipolazimika kutopata fursa ya kulala kwasababu ya kazi sikuona kama ni kero wala karaha.  

4. Ni sifa gani za pekee ambazo unadhani Kikwete anazo kama kiongozi wa nchi mwenye dhamana kubwa?

  i. Rais Kikwete amejaaliwa na Mwenyezi Mungu kutokuwa na nongwa, kutoweka visasi, na kutokuwa na chuki dhidi ya mtu yoyote hata yule aliyemtendea mabaya au kumsema vibaya. Hii inamsaidia sana kutafakari mambo na kufanya maamuzi bila kuzongwa na hisia hasi kuhusu watu au matukio. Kwa kiongozi wa nchi hili ni jambo muhimu sana. Ndio maana katika utawala wake kumekuwepo na uhuru mkubwa wa watu na vyombo vya habari kuikosoa Serikali, kwasababu suala la watu kukosoa yeyé halimsumbui. ii. Pia, Rais Kikwete ni kiongozi mtumishi. Anazunguka nchi nzima, bila kuchoka, kuwafuata watu kule waliko ili kuwasikiliza, kujua shida zao na kuzitatua. Ana bidii kubwa ya kazi na ana stamina ya ajabu, ambayo hata baadhi ya watu nusu ya umri wake hawaifikii. iii. Ni kiongozi msikivu. Anapenda kujua mambo kwa kina. Kwenye mikutano yake anatoa fursa kwa watu kuzungumza kuhusu matatizo yao, na kuuliza maswali. Ameacha simu yake wazi ili aweze kujua nini kinaendelea, aweze kusikia moja kwa moja kutoka kwa watu. iv. Anathamini sana utafiti, ili afanyapo maamuzi yatokane na tarifa sahihi.

  5. Je kuna uhusiano wowote wa kuwa kwako msaidizi wa Rais Kikwete na ukweli kwamba wewe ni mtoto wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusufu Makamba?

  Rais Kikwete aliponiteua kuwa Msaidizi wake, tarehe 21 mwezi Januari 2006, Mzee Makamba alikuwa bado hajawa Katibu Mkuu wa CCM (ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mwezi Juni 2006). Kwahiyo labda ungeuliza kwamba kuna uhusiano wowote kwa Mzee Makamba kuwa Katibu Mkuu kwasababu mimi ni Msaidizi wa Rais. Hata hivyo, dhana iliyomo kwenye swali lako kwamba Rais Kikwete anaweza kufanya uteuzi wa msaidizi wake mmoja kwasababu tu ni baba au mtoto wa msaidizi wake mwingine haina msingi, na inaashiria kutoelewa jinsi Rais Kikwete anavyofanya kazi na anavyofanya maamuzi. Rais Kikwete anateua watu kwa sifa zao na uwezo wao. Kama huko mbele baadhi yao wanamuangusha, huo ni mjadala mwingine.  

6. Katika siku na miaka ya hivi karibuni umeibuka msamiati maarufu katika vyombo vya habari na katika jamii wa ‘watoto wa vigogo’ ambao unahusisha mafanikio ya kimaisha, kikazi na kidhamana ya watu wa aina yako na viongozi wa juu ambao ni wazazi wao. Unalisemeaje hili?

  Cha msingi cha kutazama ni kama hao wanaoitwa “watoto wa vigogo” wana sifa za kushika dhamana walizonazo. Jambo la msingi ni kwamba hao wanaoitwa “watoto wa vigogo” wasipendelewe kwa kupewa kazi na dhamana ambazo hawana sifa za kuzishika kwasababu tu ni “watoto wa vigogo”, lakini vilevile wasinyimwe haki ya kupata kazi na kupewa dhamana zinazolingana na sifa zao kwasababu tu ni “watoto wa vigogo”. Bahati mbaya sana ipo dhana kwamba ukishakuwa unatoka kwenye familia ya siasa, basi mafanikio yako binafsi, ambayo umeyapigania kwa jasho lako, yanaonekana sio ya kwako, inaonekana kwamba lazima umebebwa. Baadhi yetu tunaoitwa “watoto wa vigogo” tumeishi maisha ya kawaida, tumechunga mbuzi, tumepata kuwa na funza miguuni, tumesoma shule za kawaida za Serikali hapa nchini na tumesota kweli hadi kumaliza shule na kutafuta kazi kwasababu hata hao vigogo wenyewe wapo wengi tu ambao wanapenda watoto wao wafanikiwe kwa jasho lao wenyewe. Halafu kuna hii dhana kwamba sasa nchi inaingia kwenye uongozi wa kurithishana kwasababu tu kuna vijana wanaotoka kwenye familia za siasa ambao wameamua kuingia kwenye siasa. Dhana hii haina msingi ukitazama hali halisi. Kwanza, naamini zaidi ya asilimia 95 ya wanasiasa wa Tanzania wa sasa hivi hawajatokea kwenye familia za siasa na wazazi wao hawakuwa kwenye siasa. Pili, naamini zaidi ya asilimia 95 ya wanasiasa waliopo sasa wasingependa kuona watoto wao wanaingia kwenye siasa kwasababu wao wameshaionja shubiri yake. Tatu, vijana wengi wanaoitwa “watoto wa vigogo” ambao wameamua kuingia kwenye siasa hawakusukumwa na wazazi wao. Vijana wengi siku hizi wana uhuru wa kujiamulia wanataka kufanya nini na maisha yao. Na kama wakiamua kuingia kwenye siasa basi wasishambuliwe au kusakamwa kwasababu tu wazazi wao nao wamo au walikuwemo kwenye siasa.

  7. Ziko taarifa zinazoonyesha kuwa, umeanza kujiandaa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, habari hizi zina ukweli gani?

  Ninalo wazo la kuwaomba wananchi wa Jimbo la Bumbuli wanichague kuwa mwakilishi wao.

  8. Iwapo ni za kweli, ni nini hasa kimekusukuma kufikiria kugombea ubunge badala ya kuendelea kumsaidia rais katika majukumu uliyonayo hivi sasa?  

Mambo makubwa manne:

  i. Hata kabla ya hili wazo la kugombea Ubunge, nilikuwa nimeanza kushauriana na familia yangu, kwamba baada ya kufanya kazi ya Msaidizi wa Rais kwa miaka mitano, pengine sasa nitafute changamoto nyingine. Lilipokuja wazo la Ubunge, nikatafakari kwamba: hivi kuna changamoto gani kubwa zaidi kama kuwa msemaji, mwakilishi, na sauti ya watu wa Bumbuli, watu ambao bado wako nyuma kimaendeleo? Nimejiridhisha kwamba, kwa niliyojifunza kwa miaka mitano ya kufanya kazi na Rais, uwezo wa kuwa mwakilishi mzuri ninao.

  ii. Kazi ya Msaidizi wa Rais ni kazi ya heshima kubwa, lakini ni kazi ambayo moja ya sifa zake kubwa ni kujua kufunga mdomo. Lakini binafsi, nimekuwa na hamu kubwa sana ya kushiriki mijadala mikubwa ya mustakabali wa nchi yetu, nimekuwa na hamu ya kutoa mawazo yangu binafsi na kuyaweka hadharani, kuyaboresha kupitia mijadala na utafiti, na kuyatumia kubadilisha hali za maisha ya watu wa kwetu. Nimeonelea kwamba nafasi ya Ubunge itanipa fursa hii.

  iii. Naamini kwamba, baada ya kufanya kazi kwa karibu na Rais Kikwete, naweza kuchukua mfano wake kuitumia siasa vizuri zaidi kuitumikia nchi yangu kwa namna pana zaidi. Naamini naweza kushirikiana na vijana wenzangu, wa CCM na wasio wa CCM, kuifanya siasa ivutie vijana wengi zaidi na ionekane kama ni sehemu ya utumishi wa umma.

  iv. Asilimia 72 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 29. Mwaka huu, vijana waliozaliwa mwaka 1992 watapiga kura. Letu ni taifa la vijana. Inabidi ifike mahali vijana sasa wajitokeze kwenye nafasi za uongozi ili sura ya uongozi wa nchi ifanane na hali halisi ya nchi. Tutakapojitokeza wachache na tukafanikiwa, hata vijana wadogo zetu nao watakuwa na hamu ya kufuatilia siasa na tutakuwa hatujawapoteza katika kujihusisha masuala ya nchi na wengine wengi nao watajitokeza kwasababu wataona inawezekana. Hata hivyo ujana peke yake sio sifa ya uongozi na uzee haumpotezei mtu sifa ya uongozi.

  9. Je kuna uhusiano wowote wa kugombea kwako na kile kinachoitwa kutumwa ama na Mzee Makamba au rais Jakaya Kikwete?

  Unapogombea na kuwaambia wapiga kura kwamba umetumwa na mtu fulani kugombea, hapo hapo wewe unakuwa umepoteza sifa ya kuwa kiongozi. Unaonekana haujiamini na hautoshi kuwa kiongozi, na wananchi wanalijua hilo.

  10. Kumekuwa na maneno ya chinichini yanayodai kuwa, umeshaanza kupita jimboni na kuwaeleza wananchi kuwa uamuzi wako wa kugombea una baraka zote za rais Kikwete na kwamba tayari unao uhakika wa kuwa waziri katika serikali ijayo. Unayaelezaje madai haya?

  Madai haya hayana ukweli. Kwanza, kama wewe ni Msaidizi wa Rais, halafu unaenda kugombea Ubunge unawaambia wapiga kura kwamba Rais kakutuma ugombee tafsiri yake inaweza kuwa kwamba Rais huyo hana imani na wewe kama Msaidizi wake, kwahiyo anakutuma ukagombee ili usiwe tena kwenye Ofisi yake. Wapiga kura sio wajinga. Kama unataka kura, husemi umetumwa na mtu, unachoweza kusema ni kwamba “nimekuja kugombea kwasababu nadhani kazi ya kutumwa na ninyi wananchi ni kubwa na ya heshima zaidi”. Vilevile, madai kwamba ninasema nina uhakika wa kuwa Waziri si ya kweli. Siwezi kukosa busara kiasi hiki. Na kama mtu unagombea Ubunge ili uwe Waziri, ujue unajitafutia ugonjwa wa moyo kwasababu unawekeza kwenye jitihada kubwa ya kupata Ubunge lakini kwenye kufikia lengo lako la Uwaziri, mafanikio yake yapo nje ya mikono yako. Hii ni sawa na kamari. Nagombea kuwatumikia wananchi wa Bumbuli. Kama Rais ataona ninafaa pia kumsaidia kwenye Serikali, nitaupokea uamuzi huo kwa heshima kubwa, lakini ni jambo ambalo mtu huwezi kukaa na kulisubiri.

  11. Ni nini hasa kilikusukuma hata ukafikia uamuzi wa kuamua kugombea ubunge mwaka huu na siyo kabla ya hapo na wala si mwaka 2015?

  Mwaka 2000, sikuwa kabisa na mawazo ya kujihusisha na siasa. Sana sana nilikuwa nadhamiria kufanya kazi kwenye mashirika yanayohudumia wakimbizi, au kwenye nyanja za diplomasia. Sababu nilizozitoa za kugombea zinahusiana na mazingira ya sasa zaidi kuliko 2015.

  12. Je uamuzi wako wa kugombea una uhusiano wowote na maono yako ya kushindwa kazi, kuchoka au kuzeeka kwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, William Shellukindo?  

Hapana. Sigombei kwasababu tu ya kutaka kumtoa mtu madarakani. Sigombea kupinga, nagombea kujenga. Nagombea kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Bumbuli. Ukweli kwamba Mbunge wa sasa kashindwa kazi, kachoka au kazeeka, wanaujua watu wa Bumbuli wenyewe, na kama atabadilisha ahadi yake ya kutogombea tena mwaka huu na kuamua kuchukua fomu, basi wananchi wa Bumbuli wenyewe watatoa hukumu yao. Lakini mimi ningependa wanichague kwa kuvutiwa na fikra zangu juu ya maendeleo ya Bumbuli na kwa kufaa kwangu, na sio kwasababu tu ya kutaka kumuadhibu Mbunge aliyepo, pamoja na kwamba haki hiyo pia ni yao.

  13. Je ni mambo gani hasa ambayo unayaona kuwa ni mambo ya msingi na mahitaji muhimu kwa wananchi wa Bumbuli ambayo unaamini unakusudia kuyapa kipaumbele iwapo utakuwa mbunge?

  Hapa naomba nizungumze kwa kirefu. Asilimia 90 ya wakati wa Bumbuli wanategemea kilimo. Hata hivyo, wakati Tanzania nzima wastani wa wakati kwa eneo ni watu 49 kwa kilomita moja ya mraba, Jimbo la Bumbuli wastani ni watu 309 kwa kilomita moja ya mraba, na wastani wa watu wanne wanalima katika hekta moja ya ardhi. Maana ya takwimu hizi ni kwamba watu wana vishamba vidogo sana, na uzalishaji ni mdogo na tija ni ndogo. Kwahiyo, ni muhimu kubadilisha hali hii. Nitashirikiana na wananchi kuhakikisha tunaongeza tija kwenye kilimo lakini vilevile tunajikita kwenye kuzalisha mazao yenye thamani kubwa zaidi, na kutafuta soko la maana la mazao ya wakulima. Katika Wilaya ya Lushoto yenye majimbo matatu, zao la chai linalimwa kwenye Jimbo la Bumbuli pekee. Lakini ukiwatazama wakazi wa Bumbuli huwezi kujua kwamba wanalima zao lenye soko la dunia. Nimejaribu kulinganisha kati ya mkulima wa chai Rungwe na yule wa Mponde, kule kwetu. Inasikitisha. Wastani wa bei ya majani mabichi ya chai kule Bumbuli ni shilingi 130 kwa kilo, wakati Rungwe ni karibu mara tano ya hiyo. Chai ni ile ile na mnada wa chai ni huo huo kule Mombasa. Wakulima wa chai Bumbuli wanatumia eneo kubwa zaidi kwa asilimia 40 kuliko wale wa Rungwe lakini tunazalisha kidogo zaidi – kwa tofauti ya kati ya kilo 200 hadi 330 za majani yaliyosindikwa kwa hekta. Utafiti wa mwaka 2008 unaonyesha kwamba asilimia karibu 20 ya mashamba ya chai yametelekezwa kwasababu wakulima hawaoni tena faida ya kulima chai. Nimeazimia kushirikiana na wananchi kupata ufumbuzi wa matatizo ya wakulima wa chai. Huduma bado ni tatizo. Wakati wa mvua barabara nyingi hazipitiki na shughuli zinasimama. Watu wanashindwa kwenye kupekeka maiti kwa mazishi au kwenye kuhudhuria harusi au maulidi kwasababu barabara muhimu, kwa mfano ya Soni-Bumbuli, hazipitiki. Mbaya zaidi ni kwamba kule kwetu mvua ni karibu kila siku. Katika jimbo zima la Bumbuli hakuna hata tawi moja la Benki. Inawezekanaje mahali watu wanalima zao kubwa kama chai, wana biashara kubwa za mboga na matunda lakini hawana hata tawi moja la Benki. Matokeo yake ni kwamba hakuna mikopo, na hakuna huduma ya kuweka fedha. Hali hii lazima ibadilike. Lushoto nzima lipo tawi moja tu la Benki. Lakini ukiangalia mahesabu ya lile tawi, pesa zinazowekwa ni maradufu ya pesa zinazokopeshwa. Maana yake ni kwamba ile Benki iko pale kukomba pesa za eneo lile, eneo la watu ambao ni masikini, bila kutoa huduma za mikopo. Hili na lenyewe nitalitazama. Kwenye elimu, bado ziko changamoto nyingi. Watoto wengi hawamalizi shule ya msingi. Mwaka huu, 2010, wanafunzi 1,286 hawakuingia darasa la saba kutokea darasa la sita, na kati hao, tofauti na sehemu nyingine nchini, wengi wao, karibu asilimia 71, ni wavulana. Lazima tumalize tatizo hili. Serikali imejitajidi kujenga shule nyingi za Sekondari. Lakini bado mahitaji yapo. Hadi sasa, wanafunzi waliopo darasa la saba ni takriban 5,548. Kama wote wataingia kidato cha kwanza, yatatakiwa madarasa mapya karibu 160 na walimu wengi zaidi, jambo ambalo haliwezekani kwa muda uliopo. Lakini tukienda na mwenendo wa hali halisi, labda asilimia 8-10 ya wanafunzi hawa, yaani wanafunzi kati ya 450 hadi 550, ndio wataingia kidato cha kwanza, na nusu ya hawa ndio watamaliza sekondari. Je, hawa wengine wanaenda wapi? Nitakaa na wananchi wa Bumbuli na kuzungumza kwa kina kuhusu yote haya. Tunapaswa kuongeza shule za Sekondari na hata zile zilizopo zinapaswa kuimarishwa ili kuwa na hadhi na uwezo wa kutoa elimu bora. Katika Jimbo la Bumbuli hatuna shule hata moja ya kidato cha tano na sita. Hili tutalirekebisha. Huduma ya afya na yenyewe bado haijawafikia wananchi wale kwa kiwango cha kuridhisha ingawa jitihada zimefanyika. Kwa kweli yapo mengi ambayo siwezi kuyamaliza kuyazungumzia yote. Lakini nimejiandaa vizuri. Nimefanya utafiti wa kina kuyajua matatizo ya Bumbuli, nimezungumza sana na watu wa Bumbuli, wazee kwa vijana, kina mama kwa watoto, wanyabiashara, viongozi wa dini, na viongozi wa vijiji na vitongoji, na wamenieleza mambo gani wanayatarajia, na mimi nimejiandaa kushirikiana nao kuyafanikisha.  

14. Wewe ni mtaalam wa kusomea masuala ya diplomasia ya utatuzi wa migogoro. Je unadhani kwa kuwa kwako mbunge utaweza kuutumia ipasavyo ujuzi ulionao?  

Ubunge ni uongozi wa watu, na hausomewi pahali na ubora wa Mbunge haupimwi kwa aina ya utaalam au taaluma aliyoisomea. Elimu yoyote, iwe ya udaktari au ualimu au uhandisi, inakusaidia kukupa nyenzo na uwezo wa kupambanua mambo, kuchambua mambo, kutafsiri mambo, kupanga mambo – na wakati mwingine kusimamia na kutekeleza mambo. Ninachojivunia ni kwamba napenda kujifunza mambo mengi, na najifunza kwa spidi kubwa. Katika miaka minne iliyopita nimejifunza sana kuhusu masuala ya uchumi, maendeleo ya jamii, kuondoa umaskini na masuala ya fedha. Yote haya nimejifunza kwa kununua vitabu na kujisomea, lakini pia kutokana na kazi yangu ambayo inanilazimisha kusoma mambo mengi sana. Naamini uzoefu wangu kama Msaidizi wa Rais, kwa kuzunguka na Rais nchi nzima mara mbili, wakati anaomba kura na baada ya kuchaguliwa, ambapo nimelazimika kusoma ripoti za maendeleo za Wilaya karibu zote nchini, ambapo nimehudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri, pamoja na mikutano mingine mingi ya kimataifa na ndani ya nchi, utanisaidia sana kuwa Mbunge mzuri. Naingia kwenye siasa nikiwa nimejifunza mengi kuhusu Serikali na jinsi inavyofanya kazi, nikiwa nimejifunza jinsi baadhi ya maeneo nchini yalivyopiga hatua za maendeleo na mbinu gani wametumia na wale ambao bado hawajapiga hatua ni mambo gani hawajafanya. Nitatumia elimu hii kushirikiana na watu wa kwetu kusukuma maendeleo mbele.

  15. Unadhani ni changamoto za namna gani za kiuongozi ambazo vijana wanaowania uongozi wa juu wa namna yako kutoka vyama tofauti vya kisiasa wanakabiliana nazo?

  Zipo changamoto kubwa tatu. Kwanza ni fedha. Lipo tatizo kubwa sana la matumizi makubwa ya fedha kwenye kuwania uongozi wa siasa nchini, tatizo ambalo bahati nzuri sana Rais Kikwete ameliona. Tatizo hili linawaathiri vijana zaidi kuliko makundi mengine kwasababu wengi wao huwa hawana fedha maana ndio wanakuwa wamemaliza shule, au ndio wanaanza maisha, au hawana biashara za kuwawezesha kupata fedha, au hawana fursa au sababu za kuwavutia watu wenye fedha kuwachangia. Tukiweka mazingira ya kisheria na kutengeneza utamaduni wa kisiasa ambapo fedha hazihitajiki sana kwenye kupata nafasi za uongozi wa kisiasa, basi vijana wengi watapata fursa. Changamoto nyingine ni maadili. Vijana wanaingia kwenye siasa lakini wakati huo huo bado wanahitaji kujenga maisha yao, kwa maana ya kuwa na mali na kujitengenezea maisha yao ya baadaye. Kwa kuwa ujira kwenye nafasi za uongozi wa kisiasa ni mdogo, ni rahisi kuingia kwenye vishawishi vya kutumia madaraka au nafasi za kisiasa kwa manufaa binafsi au ni rahisi kiongozi kijana kuwa ombaomba kwa watu wenye fedha ili kununua mabati, simenti au kupeleka mtoto shule au hospitali. Hii inasikitisha sana. Changamoto nyingine ni utamaduni. Kwenye jamii yetu, uzee unahusishwa na hekima na busara, jambo ambalo ni sahihi. Lakini hiyo haimaanishi kwamba hakuna vijana wenye hekima na busara ambao wanaweza kuaminiwa kwenye nafasi za uongozi wa juu wa nchi yetu. Kwa mfano, Marekani, nchi yenye uchumi mkubwa kabisa duniani, na ambayo Rais wake ana majukumu ya uongozi wa kimataifa pia, katiba yao inasema mtu unaweza kuomba nafasi ya Urais ukiwa na miaka 35. Hapa kwetu katiba inasema lazima uwe na miaka 40, wakati Nyerere na wenzake wote walipigania uhuru na kuchukua jukumu la kuijenga nchi yetu wakiwa chini ya umri wa miaka 40. Kwahiyo, ni muhimu vijana waaminiwe, sio wajaribiwe tu na nashukuru kwamba Rais Kikwete hili analitambua vyema.

  16. Ni nani hasa unaweza kumtaja kuwa ni mtu (au watu waliochangia) aliyechangia kukujengea chachu ya kutamani nawe uwe kiongozi siku moja?

  Nimekulia kwenye familia ya siasa lakini siku zote sikutamani kuwa mwanasiasa. Siku zote mdogo wangu, Mwamvita, ndiye tuliyekuwa tunamuona atakuwa mwanasiasa kutoka kwenye familia yetu. Lakini baada ya kufanya kazi kwa karibu na Rais Kikwete, nilihamasika sana nami kuiga mfano wake. Na, baada ya hapo, nimekuwa nasoma historia ya wanasiasa wengi maarufu duniani. Nimevutiwa sana na mfano na uongozi wa Bwana Dag Hammarskjold, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Mwalimu Nyerere bado anabakia ndio dira ya uongozi na mfano wa uongozi kwetu sote. Rais Mkapa pia namheshimu sana kwa mchango wake kwa nchi yetu, na mchango wake kwangu mimi binafsi.

  17. Unapoangalia mwenendo wa mambo nchini, unaweza kuuelezeaje uthabiti wa mfumo wa vyama vingi hapa nchini? Je unavitazamaje vyama vya upinzani na nafasi yake katika kujijengea mazingira ya kuwa mbadala wa CCM?

  Kimsingi, upinzani makini ni kwa manufaa ya nchi. Lakini upinzani hauwezi kuwepo tu kwasababu ni lazima uwepo. Nadhani vyama vya upinzani nchini vina kazi kubwa ya kujipambanua kwamba vinasimamia wapi kiitikadi na katika masuala ya msingi kwa nchi yetu. Haiwezekani kila siku chama cha upinzani kinashikia bango jambo jipya ambalo kwa wakati huo ndio habari moto kwenye vyombo vya bahari. Kwasababu kila siku habari zinabadilika, na kuja jambo jipya moto, inapofika wakati wa uchaguzi wananchi wanashindwa kung’amua misimamo ya vyama hivyo katika mambo ya msingi kwasababu vimepoteza muda wote wa miaka mitano kwa ajenda za kupita. Kama kazi ya vyama vya upinzani ni kupinga tu, na hakuna será mbadala, hakuna itikadi mbadala, hakuna hazina ya viongozi ambao watu wakiwatazama, na wakitazama historia yao, wanaona kweli wanaweza kushika madaraka ya nchi, basi sioni kama vinaweza kunawiri. Vilevile, nashangazwa sana kusikia ugomvi kwenye vyama vya upinzani kila siku baina ya viongozi. Mimi nilikuwa nadhani kwamba, kwakuwa watu wako katika upinzani, na jukumu la kujijenga ni kubwa zaidi na la haraka zaidi, umoja ungekuwa ni jambo muhimu zaidi na rahisi zaidi kuliko ndani ya Chama tawala. Lakini hali ni tofauti. Wananchi wanatazama, na wanaona kwamba hawa watu hatujawapa nchi wako hivi, je, tukiwapa nchi itakuwaje? Hili linapunguza sana sifa na nafasi ya upinzani kujijenga.

  18. Ni wanasiasa gani wa upinzani hapa nchini wanaokuvutia? Ni kwa nini hasa?

  Maalim Seif namuona ni mtu muungwana na kiongozi jasiri. Amenivutia sana hasa baada ya kuamua kwenda kwenye Uwanja wa Demokrasia pale Unguja kutangaza kumtambua Rais Karume na kutangaza utayari wa Chama chake kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa na CCM. Alifanya hivyo huku akijua kwamba wanachama na washabiki wengi wa CUF anaoenda kuwahutubia hawalipendi jambo hili, na kweli walimzomea na baadhi walifanya fujo lakini akabaki na msimamo huo huo, akatoa uongozi uliokuwa unahitajika, na leo hii tunakaribia kuandika historia mpya Zanzibar. Mzee wangu John Momose Cheyo wa UDP pia ni mwanasiasa ambaye siasa kwake sio ugomvi. Kila nikikutana naye tunakumbatiana kwa furaha. Hapingi jambo kwasababu tu ya kupinga ili kuonyesha msimamo, anapinga mambo kwa hoja, bila kudhihaki, kukejeli au kutafuta sifa asizostahili. Zitto Kabwe wa CHADEMA, tunazungumza, ni rafiki yangu, ni kijana anayeipenda nchi yake. Ismail Jussa wa CUF naye pia vilevile huwa nafanya naye mijadala na midahalo, mara kadhaa nakubaliana naye, mara kadhaa anakubaliana na mimi, na mara nyingine tunabakia kukubaliana kutokubaliana, lakini napenda kuzungumza naye kwasababu napenda mawazo yangu na fikra zangu zipate changamoto.

  19. Nakushukuru sana January, nakutakia kazi njema.

  Asante sana Absalom. Nakushukuru sana kwa fursa hii.

 

Skin 1